
JJe, biashara zinawezaje kuepuka madhara yanayoletwa na janga la Covid-19 katika utekelezaji wa makubaliano yake ya kimkataba?
TAPBDS tunatambua kwamba huu ni wakati ambao biashara nyingi zinahangaika kutafuta ufumbuzi wa masuala mbalimbali yanayosababishwa na athari za janga la Corona. Ikumbukwe kwamba kwa wafanyabiashara wengi ambao wamekua wanauza au kuhudumia biashara nyingine (B2B) kupitia mikataba, wao watakua na changamoto zaidi za kimkataba kuliko wale ambao wamekua wanauza au kuhudumia walaji moja kwa moja (B2C).
Mikataba hapa tuna maana ya makubaliano maalumu ya utoaji wa huduma husika yenye uzito wa kisheria. Ndani ya mikataba muuzaji hueleza anachopaswa kuuza, ukubwa wa bidhaa/huduma, muda wa mauziano na thamani ya huduma/bidhaa husika. Upande wa mnunuzi huainisha kukubaliana na muuzaji na huweka masharti au sifa za huduma/bidhaa itakayonunuliwa, utaratibu wa malipo nakadhalika. Huu ndio aina ya mkataba tunaozungumzia hapa.
Pamoja na uwepo wa vifungu vingi ndani ya mkataba vyenye lengo la kulinda maslahi ya pande zinazohusika, kipo kifungu kimoja Ambacho huandikwa ili kusaidia pande husika endapo kunatokea jambo lisilotarajiwa na linalokua nje ya uwezo kama ilivyo mlipuko wa janga la Corona. Kipengele hiki katika mikataba hujulikana kama Force Majeure. Kwa tafsiri rahisi kipengele hiki humaanisha tukio au madhara yasiyoweza kudhibitika ambayo yanatoa mwanya kwa anayeathirika kuomba kufanya marejeo ya utaratibu uliokubaliwa awali au kufanya maboresho katika mkataba. Hiki ndio kipengele Ambacho wafanyabiashara wanaweza kukiangalia kwa sasa na kuona kama kinaweza kuwasaidia katika kufanya mawasiliano na pande husika ili kupelekea marekebisho katika taratibu za kimkataba kutokana na ushahidi wa athari za janga la Corona katika utekelezaji wa shughuli za kimkataba.
Mwisho tunaendelea kuwakumbusha wafanyabiashara kuendelea kuheshimu majukumu yao ya kimkataba ikiwemo mikataba ya watumishi na wateja wao. Endapo utapata changamoto yoyote ya kimkataba wakati huu, ni vizuri utafute usaidizi wa kisheria kwanza kabla ya kufikia uamuzi wa kukatisha huduma.
Kwa usaidizi wasiliana nasi
Simu: +255222664619
Barua pepe: info@tapbds.com